Kaisari
From Wikipedia

Kaisari ni cheo cha mfalme mkuu. Neno la Kiswahili limetokana na lugha ya Kijerumani.
[edit] Asili ya Kiroma
Asili yake ni Julius Caesar aliyekuwa kiongozi wa Dola la Roma hadi kuuawa kwake na wapinzani mwaka 44 KK. Watawala waliomfuata walianza kutumia jina la Caesar kwa heshima yake hadi jina lilikuwa cheo.
Cheo cha Kaisari kiliendelea kutumika katika eneo la Dola la Roma ya Mashariki (Bizanti) hadi 1453.
[edit] Ulaya
Katika Ulaya yenyewe mfalme wa Wafranki Karolo Mkuu alipokea cheo cha "Caesar" au Kaisari. Baadaye wafalme Wajerumani waliomfuata Karolo Mkuu katika sehemu ya mashariki ya ufalme wake waliendelea kutumia cheo hiki cha Caesar au Kaisari.
Neno la Kaisari liliingia katika lugha ya Kiswahili wakati wa ukoloni wa Kijerumani huko Tanzania. Austria na Ujerumani zilitawaliwa hadi mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia 1918 na wafalme wenye cheo cha "Kaisari" (kijer.: Kaiser).
Vilevile mfalme wa Urusi alikuwa na cheo kilekile kilichoitwa "Tsar" kwa Kirusi, ilhali neno hili limeundwa pia kutoka kwa "Caesar".
Lugha za Kiingerezea na Kifaransa zilitumia cheo tofauti cha macaesar wa Kiroma ndicho "Imperator" (=mwenye amri, mwenye mamlaka, jemadari) kilichokuwa "Emperor" (Kiing.) au "Empereur" (Kifaransa).
[edit] Nje ya Ulaya
Kaisari ni cheo cha mfalme aliye juu ya wafalme wengine. Kutokana na uzuefu huu hata Shah wa Uajemi, Tenno wa Japani, Huangdi wa China na Negus Negesti wa Ethiopia hutajwa kwa cheo cha "Kaisari".
Malkia Viktoria alitumia cheo cha Kaisari ("empress") kama mtawala wa Uhindi tangu 1877.
Rais Jean-Bedel Bokassa alijitangaza kuwa Kaisari ("empereur") wa Afrika ya Kati mwaka 1977 akiiga mfano wa Napoleon Bonaparte aliyejiwekea taji la Kaisari ya Ufaransa mwaka 1804. Bokassa alipinduliwa 1979 na nchi kuwa jamhuri tena.
Categories: Siasa | Kaisari | Ufalme