Miaka baada ya hijra
From Wikipedia
Miaka baada ya Hijra ni hesabu katika kalenda ya Kiislamu.
Hesabu hii ni ilianzishwa miaka 17 baada ya tukio lenyewe (638 BK) kufuatana na azimio la Khalifa Umar.
Waarabu waliwahi kuwa na kalenda iliyotumia mwendo wa mwezi. Lakini hawakuhesabu miaka. Kila mwaka ulitajwa kutokana na tukio fulani. Mwaka wa kuzaliwa kwake Mtume Muhammad hujulikana "Mwaka wa Tembo" kwa sababu mwaka ule Makka ilishambuliwa na jeshi la Waethiopia lililokuwa na tembo wa kijeshi. Hata baada ya Muhammad desturi hii iliendelea. Mwaka wa Hijra wenyewe uliitwa "Mwaka wa kukubaliwa kwa safari," mwaka uliofuata "Mwaka vita vilipoamriwa," n.k.
Wakati wa Khalifa Umar haja ya kuwa na hesabu inayoeleweka zaidi ilionekana hivyo hesabu ya Hijra ikachaguliwa.
Waarabu waliendelea kuhesabu miaka ya miezi halisi ya siku 29 au 30 kufuatana na kuonekana halisi kwa mwezi. Kalenda ya kikristo hufuata jua badala ya mwezi ikitumia vipindi vinavyoitwa "mwezi" vilevile lakini havilingani na kuonekana kwa mwezi mwenyewe. Hivyo miaka ya Kiislamu ina jumla ya siku takriban 354. Mwaka huo wa Kiislamu una siku 11 kasoro siku zile 365 za mwaka wa jua katika kalenda ya kikristo. Katika mwaka 2006 BK hesabu ya hijra ni 1427.
Uajemi hutumia hesabu ya miaka ya Hijra pamoja na mwaka wa jua. Hivyo mwanzo wa 2006 BK huko Uajemi ni mwaka 1384 baada ya Hijra.