Guinea (kanda)

From Wikipedia

Ramani ya Kiingereza ya Afrika ya Magharibi, mnamo mwaka 1736
Enlarge
Ramani ya Kiingereza ya Afrika ya Magharibi, mnamo mwaka 1736

Guinea ni jina la kihistoria kwa ajili ya kanda ya kusini ya Afrika ya Magharibi kati ya jangwa Sahara na Atlantiki. Nchi zote kuanzia Senegal hadi kaskazini ya Angola zilihesabiwa kuwa "Guinea". Waandishi wa Ulaya walitofautisha "Guinea ya Juu" (Senegal hadi Kamerun) na "Guinea ya Chini" (Kamerun hadi Angola).

Lugha za Ulaya zilikuwa na majina ya kihistoria kwa ajili ya sehemu mbalimbali za pwani la Guinea ya juu: Pwani la Pilipili, Pwani la Meno ya Ndovu, Pwani la Dhahabu na Pwani la Watumwa. Majina haya yametokana na biashara kuu katika sehemu zile. Jina la "Pwani la Meno ya Ndovu" linaendelea kutumika katika nchi ya Cote d'Ivoire (Ivory Coast). Ghana lilitwa "Pwani la Dhahabu" hadi uhuru.

Jina la "Guinea" limetokana na jina la kale kwa ajili ya sehemu kubwa ya upande wa kusini ya Afrika ya Magharibi likimaanisha "nchi ya watu weusi" kwa lugha ya kiberber. Maelezo mengine yasema ni umbo la jina "Ghana" kutokana na ufalme wa kale.

Nchi za eneo hili zilishiriki katika biashara ya kimataifa kwa kuwasiliana na Afrika ya Kaskazini na dunia ya Kiislamu kwa biashara ya misafara ya Sahara lakini pia kwa kuwasiliana na Ulaya kupitia Atlantiki.

Biashara ya meno ya ndovu, dhahabu na watumwa ilitajirisha falme za pwani zilizopata nafasi ya kujenga enzi yao. Nchi hizi karibu na pwani zilikuwa ndogo kuliko falme kubwa za Sahel lakini zilikuwa na watu wengi na nguvu ya kisiasa pia kijeshi.

Vituo vya nchi za Ulaya kwa muda mrefu zilikuwa ndogo tu za kusaidia biashara kwanza ya watumwa baadaye ya mawese kwa mahitaji ya mapinduzi ya viwanda Ulaya. Mwisho wa karne ya 19 BK eneo lote liliingia katika kipindi cha ukoloni ya Kiulaya.

Jina la Guinea linatumika leo kwa ajili ya nchi tatu za Guinea, Guinea-Bisau na Guinea ya Ikweta. Linatokea tena katika kawaida ya lugha mbalimbali kama majina ya kijiografia ya kutaja "ghuba ya Guinea", "misitu ya Guinea", "nyanda za juu za Guinea" na kadhalika.

Kanda la Guinea ya Juu

Kanda la Guinea ya Chini

[edit] Mito

Kati ya mito mikubwa ya kanda Guinea kuna Niger na Kongo.

[edit] Tazama pia